Kwa mujibu wa ripoti ya kitengo cha tafsiri cha Shirika la Habari la Hawza, “Mkusanyiko wa Wanazuoni wa Jabal Amil” katika taarifa yake, kwa maneno makali zaidi ya kulaani na kuchukizwa, ulilaani hatua ya utawala unaokalia Israel ya kupitisha sheria za kunyonga wafungwa wa Kipalestina na kuiona kuwa ni ukiukaji wa wazi wa hukumu za sheria za kimataifa za kibinadamu, pamoja na dharau ya fedheha kwa mikataba yote na mila zinazolinda haki na heshima ya kibinadamu ya wafungwa.
Mkusanyiko wa Wanazuoni wa Jabal Amil uliongeza kwamba mwelekeo huu hatari hauwezi kutenganishwa na mienendo ya mara kwa mara ya kiuvamizi inayotekelezwa na utawala huo unaokalia; mienendo ambayo inajumuisha ukatili uliopangwa dhidi ya raia na kulengwa mara kwa mara kwa taasisi za msaada, matibabu na kijamii—iwe ni katika Palestina au Lebanon. Vitendo hivi ni ukiukaji wa wazi wa maadili yote ya kibinadamu na sheria za mbinguni, pamoja na uvunjaji dhahiri wa haki za msingi kabisa za binadamu, yaani haki ya kuishi, usalama na huduma.
Mkusanyiko huu, ukionya juu ya hatari ya mwenendo huu unaofungua mlango wa mvutano usio na kifani na ambao unaweza kuwaweka pia wafungwa wa Kilebanon katika magereza ya wavamizi katika hatari, ulisisitiza kwamba sera hizi za kikatili ni tishio la moja kwa moja kwa eneo zima na zinaweka jamii ya kimataifa mbele ya wajibu wake wa kimaadili na kisheria.
Mkusanyiko wa Wanazuoni wa Jabal Amil ulionyesha masikitiko na mshangao mkubwa kutokana na kuendelea kwa ukimya na uzembe wa serikali nyingi za Kiarabu na Kiislamu, pamoja na ukosefu wa misimamo thabiti kutoka kwa Umoja wa Nchi za Kiarabu na Shirika la Ushirikiano wa Kiislamu, pamoja na taasisi za kimataifa zinazohusika na haki za binadamu; taasisi ambazo zina wajibu wa kutekeleza nafasi yao katika kuzuia ukiukaji huu na kuumaliza.
Mkusanyiko wa Wanazuoni wa Jabal Amil ulitangaza kwamba unakataa kwa uthabiti sheria hii ya kidhalimu na kuiona kuwa ni uhalifu wa wazi unaohitaji kufuatiliwa na kuwajibishwa kimataifa.
Mkusanyiko huu pia ulilaani mashambulizi ya kinyama dhidi ya raia na kulengwa kwa hospitali pamoja na taasisi za msaada na kijamii katika Palestina na Lebanon, na ukatoa wito wa kuchukuliwa hatua za haraka na za dhati za Kiarabu na Kiislamu kukabiliana na sera hizi na kuzisimamisha kwa kutumia njia zote halali.
Mkusanyiko wa Wanazuoni wa Jabal Amil uliiitaka serikali ya Lebanon kulifanya suala la wafungwa wa Kilebanon katika magereza ya wavamizi kuwa kipaumbele cha juu kabisa, na kuchukua hatua kwa kutumia nyenzo zote za kisiasa na kisheria kwa ajili ya kuwaachilia na kulinda haki zao.
Mkusanyiko huu pia uliyataarifu mashirika ya kimataifa kuchukua jukumu lao na kuanzisha mifumo ya uwajibikaji kwa mujibu wa sheria za kimataifa, na kusisitiza kwamba kuendelea kwa uhalifu huu chini ya kivuli cha ukimya wa kutiliwa shaka wa kimataifa ni tishio la moja kwa moja kwa maadili ya haki na ubinadamu, na ni ishara ya milipuko zaidi katika eneo hilo.
Maoni yako